Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mara ya kwanza
amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho.
Magufuli
pia amekutana na wafanyakazi wa CCM Makao Makuu katika Ofisi za Chama
hicho Mjini Dodoma ikiwa ni siku tano tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti
wa Tano wa Chama hicho.
Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amekutana na watendaji hao wa CCM kwa
lengo la kuwasalimia, kupokea maoni na ushauri wao juu ya utendaji kazi
ndani ya Chama.
Katika
mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amewapongeza watendaji wote wa Chama Cha Mapinduzi kwa kazi
kubwa wanayoifanya na kwa namna ya pekee kwa jinsi walivyotoa mchango
mkubwa kuhakikisha CCM inapata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana.
Pia
amewataka kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa lengo la
kuendelea kukiimarisha Chama hicho ambacho kimebeba dhamana ya kuongoza
Serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Dkt.
Magufuli amewahakikishia kuwa chini ya uongozi wake atafanyia kazi
changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa CCM ikiwemo maslahi
duni, vitendea kazi na kuondoa utegemezi.
Aidha,
Dkt. Magufuli amewataka watumishi wa chama kutoa ushirikiano katika
zoezi la uhakiki wa mali za Chama litakalosimamiwa na sekretarieti ya
chama na ameahidi kuwa atahakikisha mapato yatokanayo na vyanzo vya
mapato vya chama yanatumika ipasavyo.
Kwa
upande wao watumishi wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho
Ndugu Abdulrahaman Kinana wamempongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
kwa kuchaguliwa kwa asilimia mia moja na wajumbe wa Mkutano Mkuu
uliofanyika tarehe 23 Julai, 2016 Mjini Dodoma kuwa Mwenyekiti wa Chama
hicho Taifa.
Watumishi hao wamemuahidi kuendeleza utumishi uliotukuka na wameelezea matumaini yao ya kuboreshewa maslahi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.